“Faida za kuitumia Damu ya Yesu kwa Imani”.
Faida ya 1 ni hii: Unapata fursa ya kuiweka kwenye matendo hiyo imani uliyonayo juu ya damu ya Yesu.
Usipoitumia ipasavyo fursa unayopata, ili kuiweka imani yako kwenye matendo, utajikuta umepoteza mambo muhimu sana, ambayo yangekuwa msaada mzuri kwa maisha yako.
Hebu tujifunze zaidi kwa kuangalia mifano ifuatayo:
Mfano wa 1: Yakobo 2:14 inasema hivi: “yafaa nini, mtu akisema anayo imani, lakini hana matendo ? Je! imani yaweza kumwokoa?”
Hii ina maana ya kuwa, ukijikuta katika vita na shetani – unahitaji kuiweka imani yako kwenye matendo, ili uweze kushinda hiyo vita! Ukiwa na imani, lakini huna matendo yanayoendana na imani uliyonayo, shetani atakushinda.
Lakini uwe na uhakika ya kuwa, utaweza kumshinda shetani, ikiwa imani yako itaambatana na matendo yadhihirishayo imani uliyonayo!
Mfano wa 2: “Imani isipokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake ….imani pasipo matendo haizai” (Yakobo 2:17, 20).
Hii ina maana ya kwamba, imani ni kama mbegu, kwa sababu hiyo kuna kitu imebeba ndani yake! Imani pasipo kuambatana na matendo, yanayoendana na kilichobebwa ndani yake, ni sawa na mbegu iliyokufa “nafsini mwake”!
Na kwa ajili hiyo imani hiyo haiwezi kuzaa! Kama vile ambavyo mbegu iliyokufa isivyoweza kuota na kuzaa!
Matendo yanayoambatana na imani, yanatengeneza mazingira ya imani hiyo “kuzaa”, kilichomo ndani ya neno, lililoweka imani hiyo ndani ya mtu! Hii ni kwa sababu “imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17).
Mfano wa 3: Yakobo 2:24 inasema ya kwamba: “mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake”.
Hii inatupa kujua ya kuwa “haki” ya kupewa kile kilichobebwa na imani, inategemea imani hiyo inavyodhihirishwa kwa “matendo”, yanayoambatana nayo!
Ni vizuri ukatofautisha kati ya “matendo ya imani” (Yakobo 2:14, 17, 20, 24, 26); na yale “matendo ya Sheria” (Rumi 3:28)!
Na pia ni muhimu ukatofautisha kati ya “sheria ya matendo”, na ile “Sheria ya imani” (Warumi 3:28).
Wakati wa agano la kale, watu walihesabiwa haki kwa “sheria ya matendo”, iliyoambatana na “matendo ya sheria”.
Lakini – wakati huu wa agano jipya, watu wanahesabiwa haki kwa “Sheria ya imani”, iliyo katika Yesu Kristo, inayoambatana na “matendo ya imani”!
Ni vizuri ujue ya kwamba, kwa njia ya imani iliyo hai – yaani iliyoambatana na matendo ya imani hiyo, unahesabiwa “kupokea” haki, iliyomo ndani ya neno la biblia lililokupa imani hiyo moyoni mwako!
Mfano wa 4: Biblia inasema katika 1 Yohana 5:4 ya kwamba “…huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu”.
Kwa mantiki ya mstari huu wa 1 Yohana 5:4, ushindi dhidi ya vishindanavyo na wana wa Mungu hapa ulimwenguni, unatokana na imani!
Lakini kufuatana na Yakobo 2:20, tunajua ya kuwa “imani pasipo matendo haizai”. Hii ina maana ya kuwa, imani pasipo matendo haina “matunda”, au haina “matokeo” yanayotarajiwa kufuatana na Waebrania 11:1.
Ikiwa unataka kuona matokeo, au unataka kuona matunda ya imani yako, yenye kukupa kuushinda ulimwengu, usisahau kuambatanisha imani hiyo na matendo stahiki.
Mfano wa 5: Je, unakumbuka mstari huu wa Waebrania 11:6? Mstari huu unasema hivi: “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu); kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”.
Mungu anapoiona imani kwako, anapendezwa na wewe! Je, unajua matokeo ya Mungu kupendezwa na wewe kwa sababu ya imani uliyonayo?
Matokeo yake ni uwepo wa Mungu kuwa na wewe! Hiki ndicho Yesu alichosema kwenye Yohana 8:29 aliposema hivi: “Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo”
Haya maneno “……nafanya siku zote yale yampendezayo” – yana maana ya kwamba siku zote anaenenda kwa Imani! Na Matokeo yake, ni uwepo wa Mungu kuwa pamoja naye wakati wote.
Imani kwenye Damu ya Yesu, bila kuitumia kimatendo – unapoteza fursa muhimu zinazoendana na imani inapotumika! Usitumie Damu ya Yesu kimazoea, wala kidini, bali itumie kwa imani itokanayo na neno la Mungu katika biblia.
Mungu azidi kukubariki tunapoendelea kujifunza juu ya Somo hili linalohusu faida za kuitumia damu ya Yesu kwa imani!
BY

No comments:
Post a Comment